WATUMISHI WANAWAKE WA TUME WAADHIMISHA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI KWA KUWAFARIJI WAFUNGWA WANAWAKE SEGEREA
Bi. Agnes Bhwana, Katibu Msaidizi (watano kulia) akikabidhi mahitaji mbalimbali kwa wafungwa wanawake wa Gereza la Mahabusu Segerea jijini Dar es Salaam wakati wa ziara iliyofanyika tarehe 06 Machi, 2026 katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani.
Watumishi wanawake wa Tume ya Pamoja ya Fedha walishiriki katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika katika Viwanja vya Barafu, Mburahati jijini Dar es Salaam. Katika maadhimisho hayo, walishiriki katika maandamano pamoja na wanawake kutoka taasisi mbalimbali za umma na binafsi, wakionesha mshikamano katika kuenzi mchango wa wanawake katika maendeleo ya jamii.
Maadhimisho ya mwaka huu, hayakuishia katika kushiriki sherehe pekee. Mapema tarehe 6 Machi 2026 walitembelea Gereza la Mahabusu Segerea jijini Dar es Salaam ambako walikutana na wafungwa wanawake na kuwakabidhi mahitaji mbalimbali kama ishara ya mshikamano, faraja na kujali wale waliopo katika mazingira magumu.
Ushiriki huo unaonesha dhamira ya Tume ya Pamoja ya Fedha katika kuunga mkono juhudi za Serikali na wadau mbalimbali katika kuimarisha nafasi ya wanawake na kuwajengea uwezo ili washiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.
Siku ya Wanawake Duniani huadhimishwa kila mwaka tarehe 8 Machi duniani kote kama jukwaa la kutambua mchango wa wanawake katika maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa pamoja na kuhamasisha usawa wa kijinsia.
Maadhimisho ya mwaka huu yamefanyika chini ya Kaulimbiu isemayo “Haki kwa Wanawake na Wasichana: Msingi wa Maendeleo Jumuishi Kufikia Dira 2050.” Kaulimbiu hiyo inalenga kuhamasisha jamii kuendelea kulinda na kuendeleza haki za wanawake na wasichana ili kuhakikisha wanapata fursa sawa katika elimu, ajira na shughuli za kiuchumi.
