MAJUKUMU
Majukumu ya Tume kama yalivyoainishwa katika Ibara ya 133 na 134 ya Katiba ni:
1. Ibara ya 133 ya Katiba
Tume inalo jukumu la kuamua kiasi cha fedha kitakachochangwa na Serikali mbili na kuwekwa katika “Akaunti ya Fedha ya Pamoja” kwa madhumuni ya shughuli za Jamhuri ya Muungano kwa Mambo ya Muungano.
2. Ibara ya 134(2) ya Katiba
a) Kuchambua mapato na matumizi yanayotokana na, au yanayohusu utekelezaji wa Mambo ya Muungano, na kutoa mapendekezo kwa Serikali mbili kuhusu mchango na mgao wa kila mojawapo ya Serikali hizo;
b) Kuchunguza kwa wakati wote mfumo wa shughuli za fedha za Jamhuri ya Muungano na pia uhusiano katika mambo ya kifedha kati ya Serikali mbili;
c) Kutekeleza majukumu mengine ambayo Rais ataipatia Tume au kama Rais atakavyoagiza, na kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge”
Aidha, kupitia Kifungu cha 124 cha Katiba ya Zanzibar ya 1984 inatambua mamlaka ya Tume ya Pamoja ya Fedha katika kutekeleza majukumu yake Zanzibar.
3. Majukumu kwa mujibu wa Sheria
Sheria ya Tume ya Pamoja ya Fedha, Sura 140 katika kifungu cha 7, imeainisha kuwa Tume itakuwa ni Chombo Kikuu cha Ushauri kwa Serikali mbili kuhusu Mfumo wa Fedha kuhusiana na Mapato na Matumizi, pamoja na fedha nyingine zitakazowekwa na pande mbili za Muungano katika Akaunti ya Fedha ya Pamoja.