WATUMISHI JFC WAASWA KUZINGATIA MTINDO BORA WA MAISHA NA KUFANYA VIPIMO KUTAMBUA HALI YA KIAFYA.
Watumishi wa Tume ya Pamoja ya Fedha waaswa kuzingatia mtindo bora wa maisha na ulaji unaofaa ili kukabiliana na athari ya magonjwa yasiyoambukiza. Aidha, wamehamasishwa kufanya vipimo mbalimbali ili kutambua hali yao ya kiafya. Hayo yameelezwa wakati wa warsha ya uhamasishaji na upimaji wa VVU, UKIMWI na magonjwa yasiyoambukiza mahala pa kazi, iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Bodi ya Sukari, Dar es salaam tarehe 20 Mei, 2024.
Akifungua warsha hiyo, Katibu wa Tume ya Pamoja ya Fedha Bw. Ernest Mchanga, aliwahimiza watumishi kusikiliza kwa makini mada zitakazowasilishwa ili waweze kujifunza. Aidha, aliwahamasisha watumishi kufanya vipimo mbalimbali ili kutambua afya zao.
Katibu wa Tume ya Pamoja ya Fedha Bw. Ernest Mchanga ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya masuala ya VVU na magonjwa yasiyoambukiza mahala pa kazi, akifungua warsha ya uhamasishaji na upimaji wa VVU, UKIMWI na magonjwa yasiyoambukiza mahala pa kazi iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Bodi ya Sukari – Dar es salaam, tarehe 20 Mei, 2024.
Dkt. Hafidhi Ameir kutoka Tume ya Kuthibiti Ukimwi (TACAIDS) akiwasilisha mada kwa watumishi wa Tume kuhusu VVU, UKIMWI na Homa ya Ini katika warsha ya uhamasishaji na upimaji wa VVU, UKIMWI na magonjwa yasiyoambukizwa mahala pa kazi, iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Bodi ya Sukari – Dar es salaam, tarehe 20 Mei, 2024.
Akizungumza wakati akiwasilisha mada kwa watumishi wa Tume kuhusu VVU, UKIMWI na Homa ya Ini. Dkt. Hafidhi alifafanua kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo umuhimu wa kupima na kupata chanjo ya Homa ya Ini, namna ya kujikinga kupata maambukizi ya virusi vya ukimwi na homa ya ini, na umuhimu wa matumizi sahihi ya kondomu za kike na za kiume, pamoja na matumizi sahihi ya dawa za kufubaza makali ya virusi vya UKIMWI mtu anapogundulika amepata maambukizi ili kuzuia virusi kuendelea kushambulia kinga ya mwili.
Dkt. Issack Lema kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili akiwasilisha mada kwa watumishi wa Tume kuhusu Afya ya akili, katika warsha ya uhamasishaji na upimaji wa VVU, UKIMWI na magonjwa yasiyoambukiza mahala pa kazi, iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Bodi ya Sukari – Dar es salaam, tarehe 20 Mei, 2024.
Dkt. Lema alieleza kuwa, Afya ya akili ni ustawi unaomwezesha mtu kukabiliana na msongo wa kila siku wa maisha na uwezo wa kukabili changamoto mbalimbali za kila siku. Alibainisha kuwa, mtu mwenye changamoto ya afya ya akili huonyesha mfadhaiko na kupoteza umakini, kuwa na uoga uliozidi na utoro kazini. Alieleza kuwa, changamoto kubwa inayowapata watu ni kutokujua namna ya kukabiliana na msongo wa mawazo hivyo hupelekea kutumia njia zisizo sahihi kukabiliana na msongo wa mawazo ikiwemo matumizi ya vilevi na ulaji usiofaa. Hivyo, aliwaasa watumishi kufanya vipimo vya afya ya akili na kuepuka kujitathmini wenyewe.
Dkt. Garvin Kweka kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, akiwasilisha mada kwa watumishi wa Tume kuhusu Uhimili wa msongo wa Mawazo, katika warsha ya uhamasishaji na upimaji wa VVU, UKIMWI na magonjwa yasiyo ambukiza mahala pa kazi, iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Bodi ya Sukari – Dar es salaam, tarehe 20 Mei, 2024.
Dkt. Kweka alibainisha sababu mbalimbali zinazosababisha msongo wa mawazo na namna ya kuepuka msongo wa mawazo. Baadhi ya mambo aliyosisitiza katika kuhimili msongo wa mawazo ni kuwa na uhusiano mzuri kazini, umuhimu wa kutenga muda na kuwa karibu na familia, kufanya ibada, kupata mtu unayemwamini na kumweleza changamoto unazopitia na kupata ushauri. Aidha, alisisitiza umuhimu wa kumuona daktari ili kupata msaada wa kitaalamu mtumishi anapopitia changamoto zinazopelekea msongo wa mawazo.
Bi. Neema Manyama, Afisa Lishe kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu, Dar es salaam akiwasilisha mada kwa watumishi wa Tume kuhusu Ulaji unaofaa na Mtindo Bora wa maisha, katika warsha ya uhamasishaji na upimaji wa VVU, UKIMWI na magonjwa yasiyo ambukiza mahala pa kazi, iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Bodi ya Sukari – Dar es salaam, tarehe 20 Mei, 2024.
Akiwasilisha mada hiyo, aliwasisitiza watumishi kuzingatia mtindo bora wa maisha na kuzingatia ulaji unaofaa ili kuepuka magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari, shinikizo la damu na magonjwa ya ini na moyo. Alibainisha sababu kadhaa zinazopelekea mtindo wa maisha usiofaa ikiwemo kuacha kula vyakula vya asili, kutopika vyakula katika njia ya asili kama kuchoma na kula vyakula vya kukaanga kwa wingi, na kutokufanya mazoezi ya mwili. Aidha alibainisha kuwa msongo wa mawazo unaweza kusababisha ulaji usiofaa, shinikizo la damu na magonjwa ya moyo.
Baadhi ya Watumishi wakifuatilia mada mbalimbali zikiwasilishwa katika warsha ya uhamasishaji na upimaji wa VVU, UKIMWI na magonjwa yasiyoambukiza mahala pa kazi, iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Bodi ya Sukari – Dar es salaam, tarehe 20 Mei, 2024.
Warsha hiyo ya siku moja iliwahusisha watoa mada mbalimbali akiwamo Dr. Garvin Kweka na Dr. Issack Lema kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dr. Hafidhi Ameir kutoka Tume ya Kuthibiti Ukimwi (TACAIDS), pamoja na Bi. Neema Manyama ambaye ni Afisa Lishe kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu, Halmashauri ya Wilaya ya Jiji la Dar es salaam.