Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Fedha

Tume ya Pamoja ya Fedha

JFC Logo
MIAKA 61 YA MUUNGANO; UHUSIANO WA KIFEDHA KATI YA SJMT NA SMZ WAENDELEA KUIMARIKA
26 Apr, 2025
MIAKA 61 YA MUUNGANO; UHUSIANO WA KIFEDHA KATI YA SJMT NA SMZ WAENDELEA KUIMARIKA

Tunapoadhimisha Miaka 61 ya Muungano wa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar uliofanyika tarehe 26 Aprili, 1964, Uhusiano wa Kifedha kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SJMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) umeendelea kuimarika.

Katika jitihada za kuendelea kuimarisha uhusiano wa kifedha kati ya SJMT na SMZ, Tume ya Pamoja ya Fedha iliundwa mwaka 2003 kupitia Ibara ya 134 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Sheria ya Tume ya Pamoja ya Fedha, Sura 140, ikiwa na jukumu la kuwa chombo kikuu cha ushauri kwa Serikali mbili (SJMT & SMZ) kuhusu masuala ya Uhusiano wa Kifedha kati ya Serikali hizo mbili ili kuimarisha Muungano wetu.

Katika maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kutoa uongozi madhubuti katika kuimarisha Uhusiano wa Kifedha kati ya serikali mbili hivyo kuzienzi ndoto za waasisi wa Muungano wetu. Uhusiano wa Kifedha kati ya SJMT na SMZ umeendelea kuimarika kama inavyobainishwa;-

Ushirikiano umeimarika katika usimamizi wa madeni na ukopaji wa nje ya nchi kwa kuzingatia vipaumbele vya maendeleo vya kila upande wa Muungano. Aidha, ushirikiano wa Serikali mbili umeendelea kuimarika katika Kamati za Usimamizi wa Madeni na Ukopaji wa Serikali nje ya nchi, zinazojumuisha wajumbe kutoka SJMT na SMZ.

Katika miaka 61 ya Muungano, ushirikiano katika upangaji wa Sera za Kodi za Muungano umeendelea kuimarika kwa kuwekwa mfumo bora wa kodi kupitia Sheria ya Bajeti Sura 439. Kila mwaka Serikali mbili zimekuwa zikishirikiana katika upangaji wa Sera za Kodi kwenye Kodi za Muungano ikiwemo Kodi ya Mapato inayolipwa na Watu Binafsi na Mashirika, Ushuru wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa Zinazozalishwa Ndani ya Nchi. Ushirikiano huo umechochea kukuza uwekezaji, biashara, na kuimarisha uchumi na ustawi wa jamii katika pande mbili za Muungano.

Sambamba na hilo, Serikali mbili zimeshirikiana katika kuwianisha viwango vya utozwaji wa kodi wa bidhaa zinazosafirishwa kutoka Tanzania Bara kwenda Zanzibar na kutoka Zanzibar kwenda Tanzania Bara. Uwiano huo umesaidia kukuza biashara, kuondoa usumbufu kwa wafanyabiashara na wananchi na umeondoa ushindani usiofaa wa kibiashara kati ya pande mbili za Muungano.

Serikali mbili zimeendelea kuimarisha ushirikiano katika kugawana mapato ya Muungano na kuchangia matumizi ya uendeshaji wa shughuli za Muungano kati ya serikali mbili.

Aidha, serikali mbili zimeendelea kufanya majadiliano ya kufikia uamuzi wa pamoja wa utaratibu wa kudumu wa kuchangia matumizi ya Muungano na kugawana mapato ya Muungano.

Katika kipindi cha miaka 61 ya Muungano, Tume ya Pamoja ya Fedha imeendelea kutoa Ushauri na Mapendekezo kuhusu masuala yanayohusu Uhusiano wa Kifedha kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili kuendelea kuimarisha Muungano wetu.