Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Fedha

Tume ya Pamoja ya Fedha

JFC Logo
SEKRETARIETI YA TUME YA PAMOJA YA FEDHA YAMUAGA MJUMBE WAKE ALIYESTAAFU
08 Jul, 2025
SEKRETARIETI YA TUME YA PAMOJA YA FEDHA YAMUAGA MJUMBE WAKE ALIYESTAAFU

Mjumbe wa Sekretarieti Bw. Ali Ali Hassan akitoa salamu za shukrani kwa Wajumbe wa Sekretarieti na Menejimenti ya Tume katika kikao kilichofanyika tarehe 29 Mei, 2025

 

Sekretarieti ya Tume ya Pamoja ya Fedha ilifanya hafla fupi ya kumuaga Mjumbe wake Bw. Ali Ali Hassan kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, baada ya kustaafu Utumishi wa Umma. Hafla hiyo ilifanyika tarehe 29 Mei 2025 baada ya Kikao cha Sekretarieti kilichojadili na kutoa maoni ya Rasimu ya Mpango Mkakati wa Tume ya Pamoja ya Fedha kwa Mwaka 2026/27 – 2030/31.

Akizungumza kwa niaba ya Sekretarieti ya Tume, Mwenyekiti wa Sekretarieti Bw. Haji Saadat alimshukuru na kumpongeza Bw. Ali Hassan kwa kuhudumu kama Mjumbe wa Sekretarieti kwa muda wa miaka kumi na nne kuanzia mwezi Mei 2011.

Bw. Saadat alieleza kuwa, katika kipindi cha utumishi wake, Bw. Ali Hassan alitoa mchango mkubwa katika kufanikisha kuimarisha Uhusiano wa Kifedha kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Sekretarieti.

Kwa upande wake, Bw. Ali Hassan aliishukuru Sekretarieti na Menejimenti ya Tume kwa ushirikiano alioupata kwa kipindi chote alichokuwa Mjumbe wa Sekretarieti. Aidha, alitoa nasaha kuhusu umuhimu wa watumishi wa umma kutekeleza majukumu yao kwa weledi. Pamoja na hilo, alisisitiza heshima na kutoa huduma kwa umma kwa usawa.

Sekretarieti ya Tume inaundwa na Wajumbe kutoka Mamlaka ya Mapato Zanzibar, Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Zanzibar, Benki Kuu ya Tanzania, Mamlaka ya Mapato Tanzania na Katibu wa Tume ya Pamoja ya Fedha.

Kwa mujibu wa Sheria ya Tume ya Pamoja ya Fedha ya mwaka 1996 Sura 140, Kifungu 11(1), inataja Sekretarieti ya Tume kuwa ni Chombo tendaji chenye wajibu wa kuchambua na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa Makamishina wa Tume kuhusu masuala mbalimbali ya Uhusiano wa Kifedha baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.