MIAKA MINNE YA RAIS SAMIA; UHUSIANO WA KIFEDHA KATI YA SERIKALI YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA NA SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR WAENDELEA KUIMARIKA
MIAKA MINNE YA RAIS SAMIA; UHUSIANO WA KIFEDHA KATI YA SERIKALI YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA NA SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR WAENDELEA KUIMARIKA
18 Mar, 2025

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anatimiza miaka minne ya Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita. Katika Uongozi wake ameendelea kuimarisha Uhusiano wa Kifedha kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SJMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).
Tunapoadhimisha miaka minne ya utekelezaji wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan, mafanikio mbalimbali katika eneo la Uhusiano wa Kifedha kati ya SJMT na SMZ yameimarishwa kama inavyobainishwa;-
Ushirikiano umeimarika katika usimamizi wa madeni na ukopaji wa nje ya nchi kwa kuzingatia vipaumbele vya maendeleo vya kila upande wa Muungano. Aidha, Ushiriki wa Serikali mbili umeendelea kuimarika katika Kamati za Usimamizi wa madeni na ukopaji wa Serikali nje ya nchi, zinazojumuisha wajumbe kutoka SJMT na SMZ.
Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuimarisha ushirikiano katika upangaji wa sera za kodi za Muungano kwa kuweka mfumo bora wa kodi kupitia Sheria ya Bajeti Sura 439. Kila mwaka Serikali mbili zimekuwa zikishirikiana katika upangaji wa Sera za Kodi kwenye kodi za Muungano ikiwemo kodi ya mapato inayolipwa na Watu Binafsi na Mashirika, ushuru wa forodha na ushuru wa bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi. Ushirikiano huo umechochea kukuza uwekezaji, biashara, na kuimarisha uchumi na ustawi wa jamii katika pande mbili za Muungano.
Serikali imewianisha viwango vya utozwaji wa kodi kwa bidhaa zinazotoka nje ya nchi na kusafirishwa kutoka Tanzania Bara kwenda Zanzibar au kutoka Zanzibar kwenda Tanzania Bara. Uwiano huo umesaidia kukuza biashara, kuondoa usumbufu kwa wafanyabiashara na wananchi, aidha umeondoa ushindani usiofaa wa kibiashara kwa wafanyabiashara kati ya pande mbili za Muungano
Katika kipindi hiki cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, elimu kuhusu uhusiano wa kifedha kati ya pande mbili za Muungano ilitolewa kwa umma kupitia maonesho mbalimbali ya kitaifa yaliyofanyika Zanzibar na Tanzania Bara, radio na televisheni. Elimu hiyo ilitolewa kwa umma wa Watanzania ili wananchi wa Zanzibar na Tanzania Bara waujue Muungano wetu na mafanikio yake.
Tunapoadhimisha miaka minne ya utekelezaji wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Tume ya Pamoja ya Fedha imeendelea kutoa Ushauri na Mapendekezo kuhusu masuala yanayohusu Uhusiano wa Kifedha kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ili kuendelea kuimarisha Muungano wetu.