Miaka 26 ya Kumbukizi ya Baba wa Taifa: Uhusiano wa Kifedha kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar umeendelea kuimarika

Katika kumbukizi ya miaka 26 tangu Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius K. Nyerere afariki dunia tarehe 14 Oktoba, 1999, Tume ya Pamoja ya Fedha inaendelea kukumbuka na kuenzi mchango wa Baba wa Taifa uliowezesha kuwa na msingi imara katika kujenga na kuendeleza uhusiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika masuala ya kifedha.
Katika kipindi cha uongozi wake, Mwalimu Julius K. Nyerere aliidhinisha na kusimamia utekelezaji wa sheria mbalimbali zilizotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo la kuwa na uhusiano imara katika masuala ya kifedha kati ya Serikali mbili.
Miongoni mwa sheria zilizoidhinishwa na kutekelezwa katika kipindi cha uongozi wa Mwalimu Nyerere ni Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada, Sura 134 ya mwaka 1974. Katika sheria hiyo, umewekwa utaratibu wa Serikali zote mbili kushirikiana katika kutafuta misaada na mikopo kutoka nje ya nchi kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa Tanzania Bara na Zanzibar. Aidha, kupitia sheria hiyo, kumewekwa taratibu zinazowezesha Serikali zote mbili kushirikiana katika usimamizi wa madeni yanayohusu ukopaji wa nje ya nchi.
Hadi sasa, ukopaji wa nje ya nchi umeendelea kufanyika kwa kuzingatia vipaumbele vya maendeleo vya kila upande wa Muungano kupitia kamati za ushauri wa ukopaji na usimamizi wa madeni ya Serikali zinazojumuisha wajumbe kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SJMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).
Katika kipindi cha uongozi wake, Mwalimu Julius K. Nyerere aliimarisha mfumo wa kodi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuidhinisha na kusimamia utekelezaji wa sheria mbalimbali zinazosimamia ukusanyaji wa kodi baada ya kutungwa na Bunge.
Miongoni mwa sheria zilizoidhinishwa na Mwalimu J. K. Nyerere ni pamoja na: Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura 332 ya mwaka 1973 (Income Tax Act, Cap 332) ambayo inatumika Tanzania Bara na Zanzibar katika usimamizi na ukusanyaji wa kodi ya mapato; Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, Sura 147 ya mwaka 1954 (Excise Duty (Management and Tarrif) Act, Cap 147) inayotumika Tanzania Bara na Zanzibar katika usimamizi na ukusanyaji wa ushuru wa bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi, na Sheria ya Forodha Na. 54 ya mwaka 1969 (kwa sasa Sheria ya Ushuru wa Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, 2004 (East African Community Customs Management Act, 2004) inayotumika katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika usimamizi na ukusanyaji wa kodi za forodha.
Sheria hizi zimeweka utaratibu wa Serikali zote mbili kushirikiana katika kufanya marekebisho ya sera za kodi ili kuweka uwiano mzuri katika kukuza uwekezaji, biashara, na kuimarisha uchumi na ustawi wa jamii katika pande zote mbili za Muungano.
Aidha, Mwalimu J. K. Nyerere aliweka utaratibu kuhusu mapato ya Serikali kuwa, mapato yote ya ndani ya Serikali yanayokusanywa Tanzania Bara yawekwe katika Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano, na mapato yote yanayokusanywa Zanzibar yawekwe katika Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Utaratibu huu umewezesha kuimarisha uhusiano wa kifedha kati ya SJMT na SMZ katika kusimamia mapato ya ndani ya Serikali. Pia, Serikali zimeendelea kushirikiana katika upangaji wa viwango vya utozaji katika kodi za Muungano: Kodi ya Mapato; Ushuru wa Forodha; na Ushuru wa Bidhaa Zinazozalishwa Ndani ya Nchi. Hadi sasa, kupitia Sheria ya Bajeti, Sura 439, ya mwaka 2015, kila mwaka Serikali mbili zimekuwa zikishirikiana katika upangaji wa Sera za Kodi.
Katika jitihada za kuendelea kuimarisha uhusiano wa kifedha kati ya Serikali mbili, katika kipindi cha uongozi wa Mwalimu Julius K. Nyerere, alianzisha Tume ya Pamoja ya Fedha kupitia Ibara 134(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, na majukumu yake yaliwekwa katika Ibara 133 na Ibara 134(2) ya Katiba.
Aidha, Tume ya Pamoja ya Fedha mwaka 2003 ilianza kutekeleza majukumu ya kutoa ushauri na mapendekezo kwa Serikali mbili yanayohusu kuimarisha uhusiano wa kifedha kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Sheria ya Tume ya Pamoja ya Fedha, Sura 140 ya mwaka 1996.
Katika kipindi cha Kumbukizi ya Kifo cha Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius K. Nyerere na katika kuenzi alama na mchango na mafanikio makubwa aliyoyaleta kwa Taifa, Tume ya Pamoja ya Fedha imeendelea kutoa ushauri na mapendekezo kuhusu uhusiano wa kifedha kati ya Serikali ya mbili ili kuendelea kuimarisha Muungano wetu.