KUMBUKIZI YA MIAKA 25 YA KIFO CHA BABA WA TAIFA

Kuimarika kwa Uhusiano wa Kifedha kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
Katika kukumbuka ya miaka 25 tangu baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius K. Nyerere afariki dunia tarehe 14 Oktoba, 1999. Katika kipindi cha uongozi wake, Mwalimu Julius K. Nyerere aliidhinisha sheria mbalimbali zilizotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Miongoni mwa sheria ziliidhinishwa ni Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada, Sura 134 ya mwaka 1974. Katika sheria hiyo, umewekwa utaratibu wa Serikali zote mbili kushirikiana katika kutafuta misaada na mikopo kutoka nje ya nchi kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa Tanzania Bara na Zanzibar.
Hadi sasa, ukopaji wa nje ya nchi umeendelea kufanyika na unazingatia vipaumbele vya maendeleo vya kila upande wa Muungano kupitia kamati za ushauri wa mikopo na usimamizi wa madeni ya Serikali zinazojumuisha wajumbe kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SJMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).
Katika kipindi cha uongozi wake, Mwalimu Julius K. Nyerere aliimarisha mfumo wa kodi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuidhinisha sheria mbalimbali baada ya kutungwa na Bunge zinazosimamia ukusanyaji wa kodi.
Miongoni mwa sheria zilizoidhinishwa na Mwalimu J. K. Nyerere ni pamoja na Sheria ya Kodi ya Mapato Sura 332 ya mwaka 1973 (Income Tax Act, Cap 332) ambayo inatumika Tanzania Bara na Zanzibar katika usimamizi na ukusanyaji wa kodi ya mapato, Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, Sura 147 ya mwaka 1954 (Excise Duty (Management and Tarrif) Act, Cap 147) inayotumika Tanzania Bara na Zanzibar katika usimamizi na ukusanyaji wa ushuru wa bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi, na Sheria ya Forodha Na. 54 ya mwaka 1969 (kwa sasa Sheria ya Ushuru wa Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, 2004 (East African Community Customs Management Act, 2004) inayotumika katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika usimamizi na ukusanyaji wa kodi za forodha.
Sheria hizi zimeweka utaratibu wa Serikali zote mbili kushirikiana katika kufanya marekebisho ya sera za kodi ili kuweka uwiano mzuri katika kukuza uwekezaji, biashara, na kuimarisha uchumi na ustawi wa jamii katika pande zote mbili za Muungano.
Aidha, Mwalimu J. K. Nyerere aliweka utaratibu kuhusu mapato ya Serikali kuwa, mapato yote ya ndani ya Serikali yanayokusanywa Tanzania Bara yawekwe katika Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano, na mapato yote yanayokusanywa Zanzibar yawekwe katika Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Utaratibu huu umewezesha kuimarisha uhusiano wa kifedha kati ya SJMT na SMZ katika kusimamia mapato ya ndani ya Serikali. Pia, Serikali zimeendelea kushirikiana katika upangaji wa viwango vya utozaji katika kodi za Muungano: kodi ya mapato; ushuru wa forodha; na ushuru wa bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi. Hadi sasa, kupitia Sheria ya Bajeti Sura 439, yam waka 2015 kila mwaka Serikali mbili zimekuwa zikishirikiana katika upangaji wa Sera za Kodi.
Katika kipindi cha uongozi wa Mwalimu Julius K. Nyerere, alianzisha Tume ya Pamoja ya Fedha kupitia Ibara 134 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, na majukumu yake yaliwekwa katika Ibara 133 na Ibara 134 (2) ya Katiba.
Aidha, Tume ya Pamoja ya Fedha ilianza mwaka 2003 kutekeleza majukumu ya kutoa ushauri na mapendekezo kwa Serikali yanayohusu kuendelea kuimarisha uhusiano wa kifedha kati ya SJMT na SMZ kuptia Sheria ya Tume ya Pamoja ya Fedha, Sura 140 ya mwaka 1996.
Katika kipindi cha Kumbukizi ya Kifo cha Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius K. Nyerere na katika kuenzi alama na mchango na mafanikio makubwa aliyoyaleta kwa taifa, Tume ya Pamoja ya Fedha imeendelea kutoa ushauri na mapendekezo kuhusu uhusiano wa kifedha kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ili kuendelea kuimarisha Muungano wetu.