KUELEKEA MAADHIMISHO YA SIKU YA KIMATAIFA YA WANAWAKE; WATUMISHI WANAWAKE WA JFC WATOA MSAADA KWA WAHITAJI
KUELEKEA MAADHIMISHO YA SIKU YA KIMATAIFA YA WANAWAKE; WATUMISHI WANAWAKE WA JFC WATOA MSAADA KWA WAHITAJI
11 Mar, 2025

Bi. Andikalo Msabila (kushoto) akikabidhi mahitaji yaliyotolewa na Watumishi Wanawake wa Tume ya Pamoja ya Fedha kwa Bi. Flora Mussa (kulia), Msimamizi wa Huduma za Kijamii katika Taasisi isiyo ya kiserikali ya Tumaini Jipya inayosaidia watoto wenye saratani Tanzania iliyopo Hospitali ya Taifa Muhimbili, walipotembelea taasisi hiyo tarehe 05 Machi, 2025.
Kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake, ambayo huadhimishwa tarehe 8 Machi kila mwaka, Watumishi Wanawake wa Tume ya Pamoja ya Fedha walitembelea Taasisi isiyo ya kiserikali ya Tumaini Jipya inayoshirikiana na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kuwahudumia watoto wenye saratani. Aidha, waliwafariji watoto wanaotibiwa katika taasisi hiyo na kukabidhi msaada wa mahitaji mbalimbali.
Bi. Lilian Nbyetabula, Msimamizi Mkuu wa Taasisi, aliwashukuru Watumishi Wanawake wa Tume kwa msaada uliowasilishwa. Aidha, alieleza kuwa uhitaji ni mkubwa hivyo aliwaomba watumishi wa Tume wawe mabalozi kufikisha taarifa ya uhitaji uliopo kwa jamii.
Akizungumza kwa niaba ya Watumishi Wanawake wa Tume ya Pamoja ya Fedha, Bi. Andikalo Msabila aliwafariji wagonjwa na kuwapongeza watumishi wa taasisi hiyo kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuwahudumia wagonjwa. Aidha, aliahidi kufikisha shukrani zilizotolewa na taasisi hiyo kwa watumishi na uongozi wa Tume.
Watumishi Wanawake wa Tume ya Pamoja ya Fedha walieleza kuwa msaada huo ni mwendelezo wa utamaduni wao wa kujali jamii na wamedhamiria kuendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali kusaidia makundi yenye uhitaji.
Siku ya Kimataifa ya Wanawake huadhimishwa tarehe 08 Machi kila mwaka, ambapo kwa mwaka huu kwa ngazi ya Taifa yamefanyika Jijini Arusha, ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.