Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Fedha

Tume ya Pamoja ya Fedha

JFC Logo
JFC YAPONGEZWA KWA KUWAJENGEA UWEZO WADAU WAKE
14 Mar, 2025
JFC YAPONGEZWA KWA KUWAJENGEA UWEZO WADAU WAKE

Dkt. Juma Mohamed Salum, Mkurugenzi wa Muungano – Ofisi ya Makamu wa Rais wa JMT akifungua Semina ya kuwajengea uwezo Wataalam kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais wa JMT, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Wizara ya Fedha ya SJMT na Ofisi ya Rais - Fedha na Mipango, SMZ, kuhusu utekelezaji wa majukumu yanayohusu mambo ya Muungano katika Wizara, Idara na Taasisi zilizo chini ya SJMT iliyofanyika tarehe 06 Machi, 2025 mkoani Morogoro.

 

Tume ya Pamoja ya Fedha iliandaa semina kwa wadau wake iliyohusu utekelezaji wa majukumu yanayohusu mambo ya Muungano katika Wizara, Idara na Taasisi zilizo chini ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Semina hiyo ilifanyika tarehe 06 Machi, mkoani Morogoro.

 

Pongezi hizo zilitolewa na Dkt. Juma Salum, Mkurugenzi wa Muungano – Ofisi ya Makamu wa Rais wakati akifungua semina hiyo akimwakilisha Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Bw. Abdallah Mitawi.

 

“naipongeza Tume kwa kuandaa mafunzo haya kwani yatasaidia kuongeza chachu ya ufanisi katika Serikali mbili na kuimarisha Muungano wetu ambao unatimiza miaka 61 ifikapo tarehe 26 aprili, 2025”, alipongeza Dkt. Salum.

 

Dkt. Salum aliongeza kuwa, “kwa hakika haya ni mafunzo muhimu sana kuweza kupatiwa watendaji wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kwakuwa taasisi zinazoshiriki katika mafunzo haya wanatekeleza shughuli za kila siku”.

 

Katibu wa Tume ya Pamoja ya Fedha, Bw. Ernest Mchanga alipokea pongezi hizo na kueleza kuwa lengo la semina hiyo lilikuwa kuwajengea uelewa wataalamu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Wizara ya Fedha ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Ofisi ya Rais - Fedha na Mipango, SMZ ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa weledi.

 

Bw. Mchanga alifafanua zaidi na kueleza kuwa, semina hiyo inakusudia wataalamu wa serikali zote mbili kuimarisha ushirikiano katika utekelezaji wa shughuli za Muungano kwa maslahi ya pande mbili za Muungano.

 

Kwa upande wake, Bw. Omary Khama, Kamishna Msaidizi wa Idara ya Usimamizi wa Madeni kutoka Wizara ya Fedha, aliishukuru Tume kwa kuendesha semina hiyo na kushauri kuwa semina hizo ziwe endelevu kwakuwa zinawasaidia watendaji kupata uelewa zaidi kuhusu masuala ya Muungano.

 

Tume ya Pamoja ya Fedha imekuwa na utaratibu wa kutoa elimu kwa wadau wake katika kila mwaka wa fedha. Miongoni mwa wadau wa Tume ni Wizara, Idara na Taasisi za Serikali zinazotekeleza mambo ya Muungano, Wananchi, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, Viongozi wa Kisiasa, Wazabuni, Watafiti na Wanafunzi.