Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Fedha na Mipango

Tume ya Pamoja ya Fedha

JFC Logo
BARAZA JIPYA LA WAFANYAKAZI LA TUME YA PAMOJA YA FEDHA LATAKIWA KUJIKITA KATIKA UTATUZI WA MIGOGORO MAHALA PA KAZI
15 Mar, 2024

Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Tume ya Pamoja ya Fedha wametakiwa kutumia Baraza hilo kama chachu ya kuleta ufanisi na tija katika utekelezaji wa majukumu ya Tume ikiwemo kutatua migogoro mahala pa kazi, badala ya kutumia muda mwingi kulalamika katika mikutano isiyo rasmi.

Kauli hiyo ilitolewa na Afisa kazi Mfawidhi, Ofisi ya kazi Dar es salaam, Bi. Vaileth Gideon Ndeza akimwakilisha Kamishna wa Kazi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Wenye ulemavu wakati wa uzinduzi wa Baraza jipya la Wafanyakazi tarehe 12 Machi, 2024 katika ukumbi wa mikutano wa Bodi ya Sukari – Dar es Salaam. ‘‘Baraza la Wafanyakazi ni chombo pekee kinachounganisha Menejimenti na Wafanyakazi kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali yanayohusu Taasisi’’ alifafanua.

Bi. Vaileth aliipongeza Tume kwa kutimiza matakwa ya sheria kwa kuwa na mkataba mpya wa kuunda Baraza la wafanyakazi, pia aliwasilisha mada kuhusu majukumu ya wajumbe wa Baraza hilo na kueleza kuwa, mabaraza ya wafanyakazi ni sehemu sahihi ya kujadili hoja mbalimbali ambazo zina vielelezo kwa ajili ya utatuzi, na uwasilishaji hoja unatakiwa uwe wa kutumia lugha ya staha. Hivyo, alisisitiza kuwa Baraza la Wafanyakazi lina nafasi kubwa katika kuleta maendeleo ya Taasisi na kuwataka wajumbe kutambua majukumu yao ili kuwatendea haki watumishi wanaowawakilisha.

Kwa upande wake Katibu wa Tume ya Pamoja ya Fedha Bw. Ernest Mchanga ambaye ndiye Mwenyekiti wa Baraza hilo, alisema “mada zitakazojadiliwa katika mkutano huo ni pamoja na Mapitio ya Utekelezaji wa Bajeti ya Mwaka 2023/2024, na Mapendekezo ya Mpango na Bajeti ya Tume kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025”. Aliendelea kufafanua kuwa, mada hizo ndiyo sababu ya msingi ya kufanyika kwa baraza hilo.

Aidha, Bw. Mchanga alimshukuru na kumpongeza Bi. Vaileth kwa kuendesha na kukamilisha zoezi la uchaguzi wa Wajumbe wa Baraza hilo na kulizindua. Vile vile, aliwapongeza wajumbe wa Baraza waliomaliza muda wao na kuwakaribisha wajumbe wapya wa Baraza.

Katika Mkutano huo, walichaguliwa, Katibu na Katibu Msaidizi wa Baraza; na Wajumbe kutoka Ofisi ya Zanzibar, Idara na Vitengo. Bw. Francis R. Daggo alichaguliwa kuwa Katibu na Bi. Nadia Mussa kuwa Katibu Msaidizi wa Baraza ambalo litadumu kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2024 hadi 2027.

Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi Bw. Ernest Mchanga (watatu kutoka kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na Wajumbe baada ya Mkutano wa Baraza. Wengine katika picha ni Bi. Vaileth Ndenza – Afisa Kazi Mfawidhi (wa nne kutoka kulia), Bw. Francis Daggo – Katibu wa Baraza (wa pili kutoka kulia) na Bi. Nadia Musa – Katibu Msaidizi wa Baraza (wa kwanza kutoka kulia). Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi ulifanyika tarehe 12 Machi, 2023 katika Ukumbi wa Mikutano wa Bodi ya Sukari, Dar es Salaam.